Na. Abel Paul, Jeshi la Polisi Mbinga Ruvuma.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limewataka madereva kuvifahamu kikamilifu vyombo wanavyotumia huku Jeshi hilo likiwataka kutambua kuwa mabadiliko ya kimifumo ya vyombo vya moto hususani mitambo hiyo mizito inahitaji mafunzo ya mara kwa mara ilikufanya wawe mahiri katika vyombo hivyo.
Hayo yamebainishwa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Marco Chilya wakati wakufunga mafunzo ya Madereva wa mitambo mizito yaliyokuwa yakiendeshwa na Taasisi ya Mitambo mizito na Teknolojia (IHET) eneo la Ruanda Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma.
Kamanda Chilya ameongeza kuwa kazi ya udereva inahitaji utulivu wa kichwa na umahiri katika kutumia chombo husika ambapo amewataka madereva hao waliopata mafunzo kutoka IHET kutochanganya mambo wakati wa matumizi ya vyombo hivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taasisi ya Mitambo Mizito (IHET) Asia Ntembu amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo madereva wa magari makubwa, maopareta pamoja na mitambo mizito huku akiweka wazi kuwa wamekuwa wakifanya hivyo katika maeneo tofauti tofauti hapa nchini ili kuwajengea uwezo.
Mkuu wa Chuo hicho amesema kuwa bila madereva makini sekta ya usafirishaji hapa nchini haitokuwa na matokeo chanya ambapo amebainisha kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikiendelea kushirikiana na Taasisi nyingine ili kuwajengea uwezo madereva.
Nao baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo licha ya kushukuru Taasisi hiyo ya IHET kwa kuwapatia mafunzo ya mitambo mizito wamebainisha kuwa mafunzo hayo yamewajengea na kuwaongezea ujunzi katika matumizi ya mitambo hiyo.